Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 22 Januari, 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi sita walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Konstantinos Moatsos – Balozi wa Ugiriki hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Fafre Camara – Balozi wa Mali hapa nchini mwenye makazi yake Addis Ababa nchini Ethiopia na Mhe. Dina Mufti Sid – Balozi wa Ethiopia hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.

Wengine ni Mhe. Elizabeth Taylor – Balozi wa Colombia hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Martin Gomez Bustillo – Balozi wa Argentina hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya na Mhe. Uriel Norman R. Garibay – Balozi wa Ufilipino mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi wote kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwapa ushirikiano utakaowezesha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi zao kukua zaidi.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Tanzania inatambua uwepo wa fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi katika nchi hizo pamoja na ujuzi na uzoefu katika nyanja mbalimbali, na kwamba ni matarajio yake kuwa ujio wao utasaidia kuongeza manufaa ya kiuchumi na kubadilishana uzoefu.

Pia Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi wa nchi zao na amewakaribisha kutembelea Tanzania.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Januari, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Balozi mteule wa Ugiriki hapa nchini Konstantinos Moatsos wakati alipokuwa akijitambulisha kabla ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Mali hapa nchini Fafre Camara Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimtambulisha Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa Balozi wa Ethiopia hapa nchini Dina Mufti Said Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Colombia hapa nchini Elizabeth Taylor mara baada ya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Argentina hapa nchini Martin Gomez Bustillo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Ufilipino hapa nchini Uriel Norman Garibay Ikulu jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...