Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itakuwa
mwenyeji wa Mkutano wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika.
Mkutano
huo utakaofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete utafanyika
tarehe 4 – 5 Septemba, 2015 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Dar es Salaam. Kauli Mbiu ni “Tumia Takwimu Huria Kuendeleza Afrika” (Developing Africa Through Open Data).
Washiriki
takriban 400 kutoka Serikalini, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Taasisi za
Elimu ya Juu na Washirika wa Maendeleo kutoka ndani na nje ya Nchi wanatarajiwa
kushiriki. Miongoni mwa washiriki kutoka
Serikalini ni pamoja na Wakurugenzi kutoka Idara za Sera na Mipango, Wakuu wa
Vitengo vya TEHAMA na Maofisa Takwimu Waandamizi wa Wizara zote.
Mkutano
wa Takwimu Huria kwa Kanda ya Afrika ni wa kwanza wa aina yake Barani Afrika Tanzania ikiwa nchi ya kwanza
kuwa mwenyeji.
Heshima hiyo imetokana na
Tanzania kujiunga na Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership – OGP)
unaolenga kuifanya Serikali kuwa wazi zaidi na hivyo kuleta uadilifu na uwajibikaji
katika kuwahudumia Wananchi.
Katika
utekelezaji wa Mpango wa OGP, Tanzania iliweka kipaumbele katika kuanzisha
Tovuti ya Takwimu Huria itakayoweka wazi takwimu mbalimbali za Serikali na
Taasisi zake.
Madhumuni
ya Mkutano ni kujadiliana kuhusu mfumo wa Takwimu Huria na jinsi utakavyoleta
maendeleo hususan kwa nchi za Afrika.
Mkutano utawawezesha wadau
kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu mfumo wa Takwimu Huria na kuona
jinsi gani Sera za nchi zenye mfumo huo zinavyofanya kazi na kusimamia viwango
vya upatikanaji wa Takwimu Huria.
Aidha, Mkutano huo
utaihusisha sekta binafsi na wadau wengine katika matumizi ya Takwimu Huria
katika kuleta maendeleo ya kasi zaidi Barani Afrika.
Washiriki watajadili jinsi ya kukuza na
kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Takwimu Huria katika kutoa huduma kwa wananchi
hasa katika sekta ya Huduma za Jamii za elimu, afya, maji na kilimo.
Tunaomba
ushirikiano wenu ili Mkutano huu ufanyike na kukamilika kwa ufanisi.
Imetolewa na Ofisi ya Rais, Ikulu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...