Na Hassan Silayo-MAELEZO
Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI)
imeendelea kuwa nguzo muhimu nchini katika utoaji wa huduma za tiba na
upasuaji.
Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo Bw. Patrick Mvungi wakati
wa Mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
Patrick amesema kuwa MOI imesaidia kuokoa zaidi ya asilimia 95 ya watanzania
ambao kwa namna moja au nyingine wangeweza kupoteza maisha yao au kupata
ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.
“MOI kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuokoa maisha ya watanzania kwa zaidi
ya asilimia 95 kutokana na kutoa huduma muhimu ya za tiba na upasuaji wa
wagonjwa wanaopokelewa na hivyo kupunguza vifo na rufaa za kuwapeleka
wagonjwa nje ya nchi” alisema Mvungi.
Akizungumzia kuhusu upasuaji wa kitaalam wa mgongo (specialized Spine
Surgeries) Mvungi alisema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kufanya na zaidi ya
asilimia 99 ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wamepona na kurudi katika hali
zao za kawaida.
Naye Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Taasisi Taasisi hiyo Bw. Almas
Jumaa alisema kuwa zaidi ya wagonjwa 1,256 ya wagonjwa wa upasuaji mkubwa
wa nyonga walipasuliwa salama na zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa hao
wamepona kabisa.
Pia Almas alisema kuwa pia Taasisi imeendelea kutoa matibabu ya magonjwa
ya ubongo yaliyokuwa yanahitaji upasuaji yamefanikiwa kufanyika kwa zaidi ya
asilimia 80 na wagonjwa waliokuwa na matatizo hayo wamepona na kuondolewa
kwenye hatari ya kupoteza uhai.
Taasisi ya MOI imewataka watanzania kuitumia Taasisi hiyo na kuacha kufuata
matibabu nje ya nchi kwa gharama kubwa tofauti na kama wangepata huduma hizo
hapa nchini kwa gharama nafuu.
Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na
Mishipa ya Fahamu (MOI) Bw. Patrick Mvungi akieleza kwa vyombo vya
habari(hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo ikiwemo kufanikiwa
kwa zaidi ya asilimia 95 ya kutoa huduma muhimu za Tiba na Upasuaji kwa
wagonjwa wanaopokelewa na hivyo kupunguza vifo na rufaa za kuwapeleka
wagonjwa nje ya nchi,wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar ea Salaam.
Kushoto ni Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Taasisi hiyo Bw. Almas
Jumaa.
Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa,
Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) Bw. Almas Jumaa akiwaeleza
waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi Taasisi hiyo ilivyoendelea kuwa nguzo
Muhimu katika kuokoa maisha ya watanzania ambapo upasuaji wa kitaalam wa
mgongo umeendelea kufanyika na kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 99 na kusaidia
kuwaondoa wagonjwa wenye tatizo hilo katika hatari ya kupotea uhai.Kulia ni
Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo Bw. Patrick Mvungi.
PICHA NA MAELEZO.
Bravo! Hongera sana! Great job!
ReplyDelete