Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeendelea kutoa elimu  kwa wakulima  pamoja na kuhakiki mizani itakayotumika kununulia zao la Pamba ikiwa ni maandalizi ya msimu wa ununuzi wa Pamba kwa mwaka huu (2018).  Zoezi hili la utoaji elimu na uhakiki wa mizani itakayotumika kununulia Pamba  linaendelea  katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Mara pamoja  na Kagera kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Vipimo Makao Makuu.

Dhumuni kuu  la utoaji elimu  kwa wakulima wa zao la Pamba  Kanda  ya Ziwa  ni kuwawezesha  wakulima  kutambua mizani iliyosahihi   (inayoruhusiwa kwa biashara)  na ile iliyochezewa (isiyoruhusiwa kwa biashara)  ili waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa vipimo wanapokuwa hawapo katika vituo vya kuuzia Pamba yao na pia ni kuwawezesha wakulima kupata  faida ya thamani kamili ya jasho lao.  
 Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Mwanza, Hemed Kipengere akitoa elimu kwa wakulima wa Pamba Wilayani Magu kuhusiana na mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kupima Pamba kwenye mizani ili Wakulima waweze kupata faida ya jasho lao la kulima Pamba.

Akizungumza na  Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano Bi. Irene John,  alisema katika maandalizi ya msimu mpya wa ununuzi wa Pamba Mwanza wanategemea kutoa elimu kwa Wilaya tano (5), Simiyu  Wilaya tano (5), Shinyanga Wilaya tatu (3), Geita wilaya sita (6), Tabora   Wilaya tatu (3) , Kagera Wilaya mbili (2) pamoja na Mara Wilaya tano (5). Hivyo, kwa mwaka huu jumla ya Wilaya 28 zimelima Pamba na zote zitapatiwa elimu  inayohusu matumizi ya vipimo sahihi  na faida zinazopatikana kwa mkulima kwa kuuza mazao yake kupitia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo.

Mwaka huu tofauti kidogo na mwaka jana maana Serikali imefufua Vyama vya Ushirika ambapo ununuzi wote wa Pamba utafanywa na Vyama vya Msingi  ambayo vinasimamiwa na wakulima wenyewe badala ya kuuza Pamba yao kupitia Mawakala kama ilivyokuwa imezoeleka miaka ya nyuma.  Mkulima wa Pamba atanufaika zaidi  kwa kuuza mazao yake kupitia vyama vya msingi sababu mazao yote  yatakayopatikana  kutoka kwenye Pamba yaani mbegu pamoja na nyuzi  mkulima atahusika kupata faida ya uuzaji wa mazao hayo tofauti na mwanzo faida kama hii ilikuwa haipatikani kwake isipokuwa kwa mfanyabiashara tu.
 Afisa wa Wakala wa Vipimo mkoani Mara wakionesha mizani sahihi na ile isiyo sahihi ili wakulima waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa wanapokuwa hawapo.

Pia kuuza Pamba kupitia vyama vya msingi itapunguza ulaghai kwenye mizani sababu wasimamizi na watumiaji wa Mizani watakuwa ni  wakulima wenyewe wa Pamba wala siyo mawakala.
 Irene  alisema Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo  kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara ikiwa ni pamoja na  kuweka   sticker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa na kukutwa kikiwa sahihi  ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.

Bi. Irene ameongezea kuwa Wakala wa Vipimo itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza  na wakawaida wakati wowote  baada ya msimu wa ununuzi wa Pamba kuanza ili panapokuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uonevu katika mizani yaweze kutatuliwa kwa haraka.
 Bi. Irene John  aliwasihi wakulima wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga kwenye Pamba kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja  ili kuleta biashara ya haki.
 Lengo kuu la Wakala wa Vipimo ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha  na siyo kupunjwa  na wafanyabiashara  wajanjawajanja.  Irene  alisisitiza kuwa kwa wale watakaobainika kuchezea mizani  kwa ajili ya kuwaibia wakulima  adhabu imeboreshwa kuanzia mwaka juzi ( Nov. 2016) hivyo, faini  itaanzia  laki moja  badala ya elfu kumi kama ilivyokuwa imezoeleka kufikia  hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa.  Kesi ikifikishwa mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...