WAKALI wa muziki wa dansi nchini Tanzania, The African Stars Band, Twanga Pepeta 'Wazee wa Kisigino', wameipania vilivyo ziara yao ya Mkoa wa Tanga, wakisema wanakwenda kuonyesha makali yao halisi kwa mashabiki wao wa muziki, kwa kuanzia na onyesho la Ijumaa Machi 23, katika Ukumbi wa Tanga Hotel, jijini Tanga kwa kiingilio kidogo tu cha Sh 7,000.

Twanga wanapanda jukwaani ikiwa ni miezi kadhaa tangu walivyoenda katika Mkoa wa Tanga, maarufu kwa Wagosi wa Kaya, jambo linaloongeza mguso kwenye shoo zao zote za Mkoa huo kutokana na kiu kubwa ya wadau wao waliokuwa na shauku ya kuiona bendi yao hiyo ikiwa jukwaani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa Twanga Pepeta, Martin Sospeter, alisema wanamuziki wao wamejipanga imara ili kudhihirisha makali yao katika tasnia nzima ya muziki wa dansi kwa kuongozwa na Luiza Mbutu, Kalala Junior, Haji Ramadhan, Msafir Diouf na wengineo wanaotamba kwenye bendi yao.

"Hakuna ubishi kuwa bendi ya Twanga Pepeta ndio alama ya muziki wa dansi nchini, hivyo ili kuonyesha umwamba huo wa kuimba vizuri, kupiga mdundo pamoja na kushambulia jukwaa, niwaombe mashabiki waje kwa wingi Ijumaa katika Ukumbi wa Tanga Hotel, kwakuwa ndio sehemu yetu ya kutangaza makali yetu.

"Mbali na onyesho la Tanga Hotel tutakaloanza mapema kabisa mishale ya saa 1 jioni, tutaendeleza dozi zetu katika Ukumbi wa Rombo Hotel Handeni Mjini siku ya Jumamosi ya Machi 24 na Jumapili ya Machi 25 tutawapa burudani mashabiki wetu wa Korogwe Mjini katika Ukumbi wa Mamba Club, huku kote viingilio vikiwa ni sh 7,000 tu," Alisema Sospeter na kuwataka mashabiki wao waende kwa wingi ukumbini kujionea umahiri wa bendi yao kongwe nchini.

Twanga Pepeta ni miongoni mwa bendi zinazotamba hapa nchini ikiongozwa na mwanamama Asha Baraka, huku ikiweza kujikita kileleni kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwake, huku ikiwa na nyimbo kali kama Mwana Dar es Salaam, Mtu Pesa, Nazi Haivunji Jiwe, Marry na nyinginezo zinazotesa katika ulingo wa muziki wa dansi nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...