Serikali imemtaka Mkandarasi Dott Services anayejenga barabara ya Mtwara-Mnivata yenye urefu wa KM 50 kwa kiwango cha lami kuongeza vifaa na kasi katika ujenzi wa barabara hiyo ili kurahisisha huduma za usafirishaji wa mazao na abiria kwa wananchi wa mkoa huo.

Akitoa agizo hilo mkoani Mtwara, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kusisitiza kuwa mkandarasi huyo anatakiwa kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaendana sawia na thamani ya fedha zilizotolewa na ubora kwa kiwango cha kisasa.

“Hakikisha unaongeza vifaa na kasi ya ujenzi wa barabara hii, la sivyo tutakutoa na hutapata kazi nyingine ya ujenzi wa barabara hapa nchini”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.Ametoa rai kwa Makandarasi wote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, weledi na kuhakikisha kazi wanazopewa zinakamilika kwa wakati na ikiwezekana hata kabla ya muda wa mkataba ili kuweza kuokoa fedha za Serikali.

Aidha ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani hapo pamoja na Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Kyongdong Engineering, kuusimamia madhubuti mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyostahili na hivyo kuweza kufungua fursa za kiuchumi na maendeleo kwa mkoa huo haraka iwezekanavyo.

Naibu Waziri huyo amesema nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri na ya uhakika kupitia miundombinu bora ya barabara vipindi vyote vya mwaka hivyo fedha za kuwalipa makandarasi zipo tayari ni jukumu lao kuikamilisha mapema.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi Dott Service na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Kyongdong Engineering wanaojenga barabara ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa KM 50 kwa kiwango cha lami na kumtaka Mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo haraka.
Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani Mtwara, Mheshimiwa Abdallah Chikota (Wa kwanza kulia), akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, (Wa pili kulia) sehemu yenye mteremko mkali katika mlima wa Nameleche uliopo katika barabara ya Mtwara-Mnivata-Tandahimba-Newala hadi Masasi yenye urefu wa KM 210 ambapo magari husumbuka katika kipindi cha mvua kutokana na mteremko huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnivata mkoani Mtwara alipofika hapo kukagua barabara ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Muonekano wa Barabara ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka Mkandarasi Dott Service, anayejenga barabara hiyo kukamilisha ujenzi wake haraka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...