Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimetakiwa kuhakikisha kwamba wanatumia vyema kijiji cha kidigitali cha Ololosokwan katika kuhakikisha kwamba taifa linakuwa na uwezo mkubwa katika tiba mtandao.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya wakati akifunga warsha ya siku 2 ya tiba mtandao iliyofanyika chuoni hapo. 

Warsha hiyo ilikuwa inakokotoa tiba mtandao ili kuwezesha mradi wa majaribio wa Tiba mtandao unaohusisha wadau mbalimbali kutekelezwa. Kitovu cha mradi huo ni kijiji cha Ololosokwan kilichopo Waso wilayani Ngorongoro. 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya akizungumza na wataalamu kutoka KCMC, MUHAS wadau kutoka The Africa Foundation, Aga Khan Foundation, Ubalozi wa Uswisi, Bill & Melinda Gates Foundation, XPRIZE pamoja na Maafisa wa afya wa mikoa na wilaya za Arusha na Ngorongoro walioshiriki kwenye warsha ya siku mbili ya tiba mtandao iliyofanyika MUHAS jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Thebeauty.co.tz)

Katibu huyo alisema kutumia kikamilifu kwa kijiji hicho hakumaanishi kuwa na majengo bali kutumia kufunza wataalamu mbalimbali kutokana na ukweli kuwa kijiji hicho sasa kitakuwa mfano wa utendaji katika kusaidia wananchi wa Tanzania. 

“Uwapo wa kijiji hiki ni tukio kubwa kwetu kwani ni kijiji cha kujifunzia, namna ya kutibu, namna ya kukusanya takwimu namna ya kubaini mahitaji na … ni mfano wa namna gani teknolojia inaweza kufanya mambo makubwa” alisema Ulisubisya . 

Alisema yeye anaamini kwamba si lazima wataalamu watiba wafundishwe eneo moja, kama ilivyo sasa, lakini wanaweza kufundishwa katika eneo kama Ololosokwan na hivyo kuwajenga pia kisaikolojia kwamba wanaweza kufanyakazi pembezoni bila ya tatizo. 
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (kushoto) akichangia jambo wakati wa kuhitimisha warsha ya siku 2 ya tiba mtandao iliyofanyika chuoni hapo. Wa pili kushoto ni mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof Ephata Kaaya (wa pili kulia) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Eligius Lyamuya (kulia).

Alisema mafanikio ya dhana ya tiba mtandao yatasaidia sana kuboresha hali ya watanzania kwa kuwa mahitaji yao yatajulikana mapema na kutokana na ukweli kuwa mradi wenyewe unahusisha pia ukusanyaji wa data wa uhakika kwa kuzingatia mahudhurio ya watu na magonjwa yao. 

Pia alisema kwa utekelezaji thabiti utaonesha namna ambavyo Watanzania tuko mbele na kusema kwamba mradi huo wa tiba mtandao anauelewa na ameupigania sana nje ya nchi ambako amekwenda kuzungumza. 

“Mwaka jana mwezi Desemba nilienda kwenye mkutano Washington unaohusu Tiba mtandao na tumeuza sana hili wazo la tiba mtandao kwa wenzetu, kwa hiyo watakuja kujifunza tunafanyaje” alisema Dk. Ulisubisya na kuongeza kwamba Wizara yake itatoa ushirikiano wa kutosha kuona dhana hiyo inatekelezeka tena kwa ufanisi. 
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi - Muhimbili (MUHAS), Prof Eligius Lyamuya (kulia) akitoa maoni wakati wa kufunga warsha ya siku 2 ya tiba mtandao iliyofanyika chuoni hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...