Wananchi wa Nakapanya, wilayani Tunduru mkoani Ruvuma  wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Nakapanya-Tunduru yenye urefu wa KM 66.5 ambayo imekamilika  kwa asilimia  Tisini na tisa na sasa mkandarasi yuko kwenye hatua za kumaliza uwekaji wa alama za barabarani.

Wakieleza furaha yao kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa mara baada ya kukagua barabara  hiyo, wananchi hao wamesema kuwa uwepo wa barabara hiyo umechochea maendeleo makubwa katika mkoa huo na mikoa ya jirani.

"Tunaishukuru sana Serikali kwani  imesikia kilio chetu cha miaka mingi cha kuomba kujengewa barabara ya lami katika wilaya yetu, sasa tunafurahia matunda ya ujenzi huu", amesema Bw. Mohammed Ally.

Kwa upande wake, Waziri Prof. Mbarawa amewataka viongozi wa Wilaya hiyo na kamati za ulinzi na usalama kuhakikisha wanawasimamia wananchi katika kuitunza na kuilinda miundombinu ya barabara hiyo ili iweze kudumu na kuweza kutumika kwa vizazi vijavyo.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumeufungua mkoa wa Ruvuma na wilaya zake pamoja na mikoa jirani ya Mtwara na nchi ya Msumbiji, hivyo kuchochea fursa za kibiashara kwa kiasi kikubwa.

Kuhusu huduma za mawasiliano  mkoani humo, Waziri Mbarawa amesema kuwa Wizara yake itahakikisha inapeleka mawasiliano haraka iwezekanavyo katika maeneo yenye changamoto hususan vijijini.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera amemhakikishia Waziri huyo kuwa  atashirikiana kwa ukaribu na viongozi wenzake katika kutekeleza maagizo yote aliyowapa ikiwemo la ulinzi wa miundombinu ya barabara hiyo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Ruvuma amemuhakikishia Waziri Prof. MBARAWA  kuwa Wakala utatatua changamoto zote zilizojitokeza wakati wa ujenzi wa barabara ikiwemo fidia kwa wananchi waliovunjiwa nyumba zao kupisha barabara hiyo.
 Muonekano wa barabara ya Nakapanya-Tunduru KM 66.5 iliyokamilika kwa kiwango cha lami, mkoani Ruvuma.
 Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Ruvuma Eng. Lazeck Alinanuswe (mwenye koti la kaki), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto kwa Meneja), ujenzi wa kingo za Daraja la Lumesule lililopo mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na Mtwara wakati alipokagua daraja hilo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisikiliza maoni kutoka kwa Bw. Mohammed Ally mkazi wa Nakapanya, Wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma kuhusu furaha yao juu ya kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya Nakapanya-Tunduru KM 66.5.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), picha ya barabara ya Nakapanya-Tunduru KM 66.5 iliyokamilika kwa kiwango cha lami wakati alipokuwa akikagua barabara hiyo, mkoani Ruvuma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera.
 Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Dua Nkurua (kushoto), akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), mara baada ya kuzungumza na uongozi wa wilaya hiyo, mkoani Mtwara.
 Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera (mwenye koti la kaki), akimuonyesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto kwa Mkuu wa Wilaya), moja ya ofisi katika jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya huyo, alipoikagua Wilayani humo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na uongozi wa Wilaya ya Tunduru, mara baada ya kukagua miradi iliyo chini ya Wizara hiyo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifurahi jambo na wafanyakazi wa kampuni ya Korosho, Wilayani Tunduru mara baada ya kutembelea na kuangalia uzalishaji wa korosho katika kiwanda hicho.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...