Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.

Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Plan International limezindua Mpango Kazi wa miaka 5 utakaowawezesha wasichana wanaoishi katika mazingira magumu kujitambua na kujisimamia wenyewe katika nyanja mbalimbali zitakazowaletea maendeleo. 

Mpango kazi huo unaanza mwaka 2017- 2022 ukiwa na lengo la kuwasaidia wasichana 1,000,000 ulimwenguni kote.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kanda ya Nchi za Afrika Mashariki na Kusini – Plan International, Roland Angerer alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malengo ya mpango kazi huo.

Angerer amesema kuwa Shirika hilo limepanga kuisaidia Serikali ya Tanzania kufikia Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 kwa sababu mpango huo umelenga kutengeneza mazingira mazuri kwa watoto hasa wasichana na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika suala zima la maendeleo.

“Plan International wameweka mpango mkakati wa ulimwengu mzima ambao utawasaidia wasichana sio tu katika kupata elimu bali kuwafanya wawe na nguvu itakayowasaidia kujifunza, kujiongoza, kuamua pamoja na kujipigania katika mambo mbalimbali yanayowahusu,”alisema Angerer.

Ameongeza kuwa usawa wa kijinsia ni moja ya Mpango wa Maendeleo Endelevu hivyo wataweka juhudi kubwa katika kuhakikisha wasichana wanapata haki sawa na wavulana kwani usawa huo utasaidia kuharakisha maendeleo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo- Tanzania, Jorgen Haldorsen amesema kuwa nchini Tanzania mpango huo utalenga zaidi katika kuzuia ndoa za utotoni kuanzia katika ngazi ya Kitaifa hadi Vijiji ili kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki zake.

”Kwa kushirikiana na Serikali , tumeanzisha miradi ya kuzuia ndoa za utotoni katika Mikoa ya Mara, Geita,Morogoro na Rukwa na katika mikoa hiyo tunategemea kuwafikia moja kwa moja wasichana 12,000 na kuwafikia wasichana 120,000 kwa njia zingine tofauti,”alisema Haldorsen.

Amefafanua kuwa pamoja na jitihada zote na rasilimali mbalimbali kuelekezwa kwenye jamii kupitia Mikoa,Wilaya na Kata lakini bado wanatambua umuhimu wa kufanya kazi na Serikali katika ngazi ya kitaifa kwa kutoa maoni na uzoefu wao katika kutengeneza sera zinazomuhusu mtoto na usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake Muhamasishaji kutoka Mradi wa Vijana wa ‘Youth for Change’, Upendo Abisai amelishukuru shirika hilo kwa kufanya jitihada katika kuhakikisha msichana anapata haki zake kwani ulimwengu mzima wasichana ndio wanaokumbwa na changamoto nyingi zinazowapelekea kutotimiza malengo yao. 

“Sisi kama vijana wa ‘Youth for Change’ tumepewa fursa kubwa ya kuwafikia na kuwaelimisha vijana wenzetu juu ya haki zao za msingi pia tuna nafasi ya kuwasemea wale ambao hawajapata nafasi ya kusema ili kuhakikisha wote kwa pamoja wanapata haki zao”,alisema Bi. Upendo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...