Na Lulu Mussa, Katavi 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema kuwa uharibifu wa Mazingira katika Mto Katuma ni tishio kubwa kwa uhai wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi na wakazi wa Mkoa huo. 
Akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya siku 16 kutembelea Mikoa mbalimbali hapa nchini, Waziri Makamba amesema kuwa Mto Kasuma uko hatarini kutoweka kutokana na ongezeko la shughuli za binadamu, wingi wa mifugo,  Uchimbaji wa madini, ukataji wa miti na uchepushaji wa maji kunakopelekea kupoteza mtiririko wa maji yenyewe. 
Waziri Makamba amesema ni vema kuwa na mikakati na hatua za haraka na zile za muda mrefu ikiwa ni pamoja na kufanya sensa ya mifugo ili kuweza kujua Mkoa una mifugo kiasi gani na kuainisha maeneo ya malisho. "Zoezi hili si hiari, ni lazima na takwa la kisheria' Makamba alisisitiza.
 Imependekezwa pia kufanyika kwa Ubomoaji wa mabanio yanayokinga maji kama hatua ya haraka ili maji yaweze kutiririka kwa wingi katika kipindi hiki cha kiangazi, na kuagiza kufanyika kwa doria za mara kwa mara ili kubaini watu wanaokiuka taratibu hizo. 
Waziri Makamba pia amezitaka Mamlaka za bonde kutimiza wajibu wao kwa kutoa vibali stahiki kulingana na ujazo wa maji uliopo katika maeneo yao ili kujenga usawa wa matumizi sahihi ya rasilimali maji. ' Mamlaka za bonde zisitoe vibali ofisini na operesheni ifanyike kwa wote wasio na vibali" Alisema Waziri Makamba. 
Pia, Waziri Makamba ameagiza kufanyika kwa Tathimini ya athari kwa mazingira kwa Mto Kasuma na kuuagiza uongozi wa Mkoa wa Katavi kuainisha baadhi ya maeneo ambayo yatatangazwa kama maeneo nyeti ili kunusuru mazingira ya Katavi na ustawi wa Mto Katuma.
"Kuwe na tozo ya uharibifu wa Mazingira na tozo hiyo iendane na kiwango cha uharibifu atakachofonya muhusika" 
Akiongea na Wadau wa Mazingira katika Ukumbi wa Maji Mkoani Katavi Waziri Makamba amekumbusha watumishi wa Umma Nchini kuwa na nidhamu na uwajibikaji wa dhati na kusisitiza kuwa hakuna muda wa kubembelezana. "Fanyeni kazi kwa weledi, nidhamu na uadilifu" alisema Makamba. 
Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametembelea eneo ulipokuwa mradi wa uchenjuaji wa dhahabu wa Jema Sitalike Project ambao ulikua ukifanya shughuli zake bila kibali cha Wizara ya Nishati na Madini na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). 
Waziri Makamba ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Mradi wa Jema ambao kwa sasa wamehamishia shughuli zao Mkoani Mwanza na kuwataka kuchukua hatua za haraka kufunika mashimo yaliyopo Sitalike - Katavi ili kunusuru uhai wa viumbe vinavyozunguka maeneo ya Sitalike. 
Waziri Makamba yuko Mkoani Katavi kwa ziara ya kikazi na hii leo amekutana na Viongozi wa Vikundi vya Mazingira, katembelea eneo lilikokuwa na shughuli za Uchimbaji wa Madini na  chanzo cha Mto Katuma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiangalia eneo lililokuwa likitumiwa na Jema Sitalike Project ambao walizuiwa kuendelea na shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kutokana na kutokuwa na vibali. Wengine katika picha ni pamoja Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga
 Mashimo yaliyokuwa yakitumiwa na Jema Sitalike Project ambao walizuiwa kuendelea na shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kutokana na kutokuwa na vibali, yakiwa yameachwa wazi hali inayotishia usalama wa wananchi wanaozuka maeneo hayo. Waziri Makamba ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Mradi wa Jema ambao kwa sasa wamehamishia shughuli zao Mkoani Mwanza na kuwataka kuchukua hatua za haraka kufunika mashimo yaliyopo Sitalike - Katavi
Viboko Katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi wakiwa wanaathirika kutokana na upungufu wa maji katika Mto Katuma. Waziri Makamba ametangaza hatua za haraka na za muda mrefu za kurejesha mto huo katika hali yake ya awali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...