WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (pichani) ameishutumu Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa ni kikwazo kwake katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha bandari ya Dar es Salaam ikiwa nipamoja na utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
 
Dk. Mwakyembe alisema watu wengi wanaoitumia bandari ya Dar es Salaam (TPA) wanalalamikia  madudu wanayofanya TRA hasa  tatizo la kufeli  kwa mfumo wa mawasiliano ya kompyuta unaotumiwa na mamlaka hiyo kutoza kodi mbalimbali.
 
Alitoa shutuma hizo baada ya kutakiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Watanzania wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika jiji la Guangzhou, jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China.
 
Jana usiku (Alhamisi, Oktoba 24, 2013)Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake ya China kwa kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi katika jimbo hilo maarufu  kwa biashara.
 
Bw. Stanley Mwakipesile ambaye ni mfanyabiashara wa  Kariakoo anayefuata bidhaa zake katika jimbo la Guangzhou, katika hoja zake alisema utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ni tatizo kubwa kutokana na mfumo wa kutoza kodi unaotumiwa na TRA kutofanya kazi siku zingine na hivyo kusababisha mteja kutozwa fedha nyingi.
 
Mfanyabiasahra huyo alisema kutokana na kero hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wameikimbia bandari hiyo na sasa wanatumia bandari ya Mombasa jambo ambalo alisema ni hasara kwa nchi. “Inakuwaje kila siku pale TRA system inakuwa down? Kuna urasimu mwingi tu pale lakini cha ajabu wakati wao ndio hawafanyi kazi, lakini mteja anatozwa eti kachelewesha kutoa mzigo,” alisema Mwakipesile.
 
Dk. Mwakyembe katika kujibu hoja za mfanyabiashara huyo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na akasema eneo linalolalamikiwa sana ni TRA ni kuwatoza wateja tozo za ziada hata kipindi ambacho watendaji wa mamlaka hiyo hawafanyi kazi kwa kisingizio cha mfumo kutofanya kazi (system down).
 
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli TRA ni tatizo,  hasa hili la system down kwa kweli ni kero na linawaumiza watu wengi wanaotumia bandari yetu. Ni lazima tukae tuone namna ya kutatua tatizo hili,” alisema Mwakyembe.
 
Alisema licha ya kuwepo agizo kutoka serikalini la kutaka TPA na TRA wafanye kazi saa 24, lakini watendaji  wa TRA wanafanya kazi kwa saa 12 tu  na wanalala kwa siku 10 katika mwezi mzima.
 
Alisema wakati TRA wanaenda kulala, mteja hahudumiwi  na wanapokuja kuendelea na kazi kesho yake,  wanawatoza  wateja tozo ya kuchelewesha mzigo wakati makosa siyo ya wateja  bali ni ya watendaji wa mamlaka hiyo ya kukusanya kodi kwa Tanzania.
 
“Sisi TPA hatulali; lakini wenzetu hawa wanalala, inakuwaje wanaenda kulala wakati mizigo imerundikana pale bandarini? Kwa kweli hawa watu ni lazima tushughulike nao.
 
“Mimi nimesaini BRN, Rais anataka kuona mwaka 2015 shehena inaongezeka pale, na kufikia tani 18 sasa yule atakayekaa mbele yangu kunikwamisha mie nitampitia,” alisema Dk Mwakyembe na kushangiliwa kwa nguvu na watanzania hao.
 
Hata hivyo aliwatoa hofu Watanzania kwa bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na kila mwaka shehena imekuwa inaongezeka, hali inayoonyesha kuwa batu nchi nyingi ikiwemo Zimbabwe bado zinatumia bandari hiyo.
  
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, OKTOBA 25, 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Tanzania inahitaji watu wenye uthubutu,najua wengi tu watakereka na kauli ya mwakyembe lakini huu ndio ukweli, watu wanakaa wanalipana vizuri kwa jasho la mlala hoi lakini huduma kwa mlala hoi huyo huyo anaewalipa zinakua mbovu, mwakyembe chukua form 2015, labda tupate mtu wa kutukemea pengine adabu itarudi kiidogo.

    ReplyDelete
  2. TRA ni janga la kitaifa mh Mwakyembe. mimi niliwahi hutuma ka mzigo kadogo sana pale Airport kwa DHL.siku ya pili mzigo ulukuwa umeshafika ila ngoma nzito ni kukatoa yaani kidogo niuache kwani wanaushikiria ili upate usumbufu na unalazimoika kusema sasa niongeze ngapi na mzigo unatoka siku hiyo hiyo.Juzi nilisoma report kuwa watanzania hutoa Rushwa wenyewe kwa polisi ila si kweli kuwa wanapenda ila usumbufu unaojengwa na watendaji wetu tunaowalipa kwa kodi unalazimisha watanzania kufikiria kutoa pesa ili mambo yaende. kwa kweli watu waliozoea nchi za watu na hata utendaji wa majirani zetu tu kama Rwanda sehemu kama TRA kucheza na maendeleo ya nchi inatia kinyaa na kichefuchefu. Mh Mwakyembe usifanye mzaha shughulika nao nasi tutakuwa nyuma yako.

    ReplyDelete
  3. Kikwete kama rais wa nchi yetu tunakuomba umsaidie huyu ndugu Mwakyembe na ikiwezekana TRA ifumulie na ijengwe upya,,chukueni maamuzi magumu kwa watu wajinga kama hao Tra

    ReplyDelete
  4. Tujifunze kwa wenzetu jamani... obamacare website imeleta kigugumizi, angalia system nzima ya serikali inavyotafuta mchawi. Sisi TRA computer system is down - causing loss to the nation, but we are muffled.

    ReplyDelete
  5. Upo China! Waandisshi elewesheni ummma vizuri!

    ReplyDelete
  6. Kwa kweli mimi najiuliza hivi kuna viongozi waliochaguliwa kurudisha maendeleoa nyuma? Au walipewa vyeo kwa kujuana? Hivi kwanini hatujifunzi toka nchi za wenzetu.wao wanakimbia sisi tunatambaa.TRA ifanyiwe mageuzi makubwa sasa kwani wamekuwa miungu watu na pesa nyingi inaishia mifukoni mwao.mwakyembe tunataka kazi uliofanya bandarini sasa ionekane pia hapo TRA.tumechoka na tutaendelea kutumia bandarini za nje mpk watakapokuwa sawa.









    ReplyDelete
  7. TRA ni tatizo sugu mimi ni mmojawapo wa walio athirika na'system down' nikatozwa storage charges si chini ya $300 wakati tatizo sio langu.Halafu mmimi na clearing agent tukafanikiwa kuingia kwenye ofisi ya hiyo ya system, basi tulikemewa hata kutaka kuitiwa polisi.Sasa kama sisi wateja tunaochangia kiasi kikubwa cha pato la taifa kunyanyaswa na kulipishwa charges ambazo ni unnecessary, kweli tutafikisha malengo ya pato la taifa? Nimekuwa nikiulizwa na wenzangu wa nchi kama Burundi,Rwanda nk ambao wangependa kuendelea kutumia bandari yetu lakini wanakwamishwa na 'usingizi' wa TRA.Mh.Mwakyembe, hivi huyo waziri husika wa hao TRA bado nae yuko usingizini hata haamshwi na kilio chako cha siku nyingi juu ya usingizi wa TRA?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...