Na Mwandishi Wetu. 
KAMPUNI ya Camel Oil  imesema uuzwaji wa kiwanja namba 130 kilichoko Block A, Manzese jijini Dar es Salaam ulizingatia taratibu zote za kisheria na kwamba hakuna sehemu iliyoghushi hati za kiwanja hicho kama inavyodaiwa.

Akizungumza na jijini Dar es Salaam, Meneja wa Kampuni hiyo, Mahfoudh Ally, alisema kampuni yake ilifata taratibu zote za kiubinadamu na kisheria katika kuuza kiwanja hicho baada ya mmiliki wa awali, Mzee Mohamed Fakhi kushindwa kulipa deni la Sh bilioni 1.4.

Amsema ameamua kuweka wazi suala hilo baada ya  kuona utitiri wa habari za nia ya kupotosha ukweli.

Mahfoudh kuuza kiwanja hicho ulikuwa uamuzi wa mwisho kabisa baada ya jitihada za muda mrefu zilizogonga mwamba baada ya ahadi hewa nyingi sana kutoka kwa mdaiwa  Mzee Mohammed.

Amesema kabla ya mwaka 2010 kampuni yake ilifanya biashara kwa muda mrefu na Mzee Mohamed  wa Manzese Filling Station kuhusiana na  kuuza  mafuta kwa mkopo kwa makubaliano kwamba Camel Oil ilipwe kila mwisho wa mwezi.

Mahfoudh amesema Camel Oil iliendelea kukipa kituo hicho mafuta lakini mmiliki wa kituo hicho aliendelea kulimbikiza deni hadi kufikia Sh bilioni 1.6 na mwaka 2012 aliacha kununua mafuta kwenye kampuni hiyo ya Camel bila kutoa taarifa yoyote, na Mzee Mohammed pamoja na mtoto wake wakatokomea kusikofahamika.

“Tulifuatilia kujua kwanini kulikuwa na ukimya wa muda na tulitaka kujua atalipaje deni hilo, baada ya kumtafuta tulimpata na tukakubaliana namna ya kulipa deni hilo. Alitoa hundi ambazo baadhi zilipita na nyingi ziligonga ukuta kwani hakuwa na hela benki. Kwa mara nyingine akatokomea kusikojulikana.  Jitihada za dhati ziliendelea kumtafuta na kumsihi alipe ila palikuwa na kila dalili ya kushindwa kulipa deni. Na tulipoona anashindwa kulipa deni tuliomba kushikilia hati mbili za viwanja vyake kama dhamana,” alisema.

Amesema, Mzee Mohamed alikubali mwenyewe kwa maandishi kwamba viwanja vyake vishikiliwe na Camel Oil kama dhamana ya deni hilo analodaiwa, na ushahidi wote wa maandishi upo.
“Kwa masikitiko Makubwa, Camel tulibaini baadaye kuwa hata viwanja wanavyotaka kuchukua kama dhamana, Mzee Mohamed alishaviweka dhamana kwenye kampuni zingine ambazo zinamdai madeni mbalimbali,” alisema.

amesema kuwa hati moja ya kiwanja cha kitalu A, kilichopo Manzese ilikuwa inashikiliwa na Kampuni ya TOTAL  iliyokuwa ikimdai Mzee Mohamed Sh.milioni 165 lakini Camel Oil ilikubali kulipa deni hilo ili kushikilia hati hiyo kwa makubaliano na Mzee Mohamed kwamba fedha hizo ziongezwe kwenye deni la awali la Sh. Bilioni 1.6, ambazo Camel Oil inamdai. Pia ushahidi wa maandishi upo.

Mahfoudh alisema kwenye mkataba wa kukubali deni iliyosainiwa Septemba mwaka 2010, Mzee Mohamed alikiri kudaiwa na Camel Oil Sh bilioni 1.6 ambazo alikubali kuzilipa kwa mujibu wa masharti na makubaliano kwenye mkataba huo, kitu ambacho hakuonyesha dalili ya kutekeleza alichokiahidi.

Mahfoudh alisema kwenye makubaliano ya mkataba huo, Mohamed ambaye ni mdaiwa alikubali kuweka dhamana kiwanja namba 130 Kitalu A Manzese chenye thamani ya Sh milioni 850 na kiwanja namba 861 na namba 862 cha Msasani Beach vyenye thamani ya Sh. 300,000,000.

“Katika hatua isiyo ya kawaida na ya ajabu, ya kusikitisha na kudhalilisha, hasa kwa mtu mzima kama Mzee Mohammed, ni kwenda kula kiapo Polisi pamoja na Ardhi kwamba alipoteza hati za viwanja vyake akiwa na nia mbaya ya kudhulumu, kufisadi na kuidanganya Serikali mchana kweupe. Hiki kilikuwa kitendo kibaya na cha kitapeli. Nyaraka zote za ushahidi pia zinaonyesha kila kitu kinagaubaga,” alisema Mahfoudh.

“Kweli ukistaajabu ya Musa, uatayaona ya Firauni. Kama vile hii haitoshi, baada ya kugundulika njama zake , Mzee Mohammed alifungua kesi ya kughushi, dhidi ya Camel Oil. Baada ya muda sio mrefu, Mzee Mohammed alikiri mwenyewe kufuta kesi ya kughushi na akamuandikia barua IGP na DPP na Camel wakapata nakala. Katika barua yake, anasema aliamua kufuta kesi ya kughushi, bila ya kushurutiswa na yeyote, ila pengine nafsi ilimsuta,” alisema.

Mahfoudh alisema baada ya jitihada zote kufanyika ili Mzee Mohamed alipe deni hilo ilishindikana na ndipo walipomtafuta dalali kwa ajili ya kuuza kiwanja cha Manzese kujaribu kufidia deni ambalo wanamdai.

Alisema Kampuni ya Udalali ya Bilo Star Debt Collectors ilipewa kazi hiyo na tarehe 3 Julai ilitoa tangazo kwenye gazeti la Mzalendo kwa ajili ya kuuza kiwanja cha Mzee Mohamed kilichoko  Manzese kama sehemu ya kufidia deni analodiwa na taratibu zote za msingi na kisheria zikawa zimezingatiwa.

“Ingawa tulijua hata tukiuza kiwanja kile hatutapata kiasi tunachomdai ambacho kwa mwaka 2016 kilishapungua na deni mpaka Julai 2016 lilikuwa Sh. Bilioni 1.4 lakini tuliamua tu tuuze angalau tupate kitakachopatikana kuliko kukosa kabisa maana mdaiwa alionyesha dalili zote za kushindwa kulipa deni,” alisema.

Aidha, alisema mnada wa hadhara ulifanyika tarehe 9 Julai 2016 na Kampuni ya State Oil ndiyo ilipata kiwanja hicho kwa kununua kwa Sh bilioni moja (1,000,000,000) hivyo kuwa mmiliki halali wa kiwanja hicho namba 130, Block A Manzese jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...