Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Juni, 2016 amezindua kituo cha mawasiliano cha Jeshi la Polisi ambacho kitarahisisha utoaji wa taarifa za uhalifu na kuharakisha askari polisi kufika katika eneo la tukio.

Kituo hicho cha kwanza kuanzishwa na Jeshi la Polisi hapa nchini kipo katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam na kinafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu na mfumo wa utambuzi wa eneo (GPS) ambapo askari polisi waliopo katika kituo cha mawasiliano watakuwa wakipokea simu kutoka kwa wananchi wanaotoa taarifa za matukio ya uhalifu na kisha kuwaelekeza askari walio jirani ili wafike eneo la tukio na kukabiliana na wahalifu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu amemueleza Rais Magufuli kuwa kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 18 kwa mpigo kutoka kwa watu wanaopiga simu ya bure namba 111 au 112 kwa ajili ya kutoa taarifa za uhalifu na kwamba lengo la jeshi hilo ni kuhakikisha askari wanafika eneo la tukio ndani ya dakika 15.

IGP Mangu ameongeza kuwa kituo hicho kimeanzishwa kwa msaada kutoka benki ya CRDB iliyotoa shilingi milioni 320, kitaanza kutoa huduma tarehe 01 Julai, 2016 kikianzia katika mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Kanda maalum ya Dar es salaam na polisi imejiwekea malengo ya kuwa na vituo kama hivyo nchi nzima ifikapo mwaka 2019. 

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha mradi huo na ameahidi kuwa serikali itahakikisha inaunga mkono mpango huo ikiwa ni pamoja na kulifanyia kazi ombi la kununuliwa helkopta itakayorahisisha zaidi ufikaji eneo la tukio. 

Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kuwanyang’anya silaha wahalifu kabla hawajawadhuru raia na kupora mali zao ama kusababisha mauaji, na amewataka viongozi wa jeshi hilo kuwazawadia askari wanaofanya kazi nzuri ya kupambana na wahalifu. 

Dkt. Magufuli pia ametaka jeshi la polisi lisimame imara kuhakikisha serikali inatekeleza ahadi zake kwa wananchi zikiwemo upatikanaji wa maji na huduma nyingine za kijamii na kwamba hatarajii kuona mtu yeyote anafanya vitendo vitakavyosababisha ahadi hizo kutotekelezwa. 

Katika hatua nyingine, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuiongoza nchi. 

Mufti Mkuu Sheikh Aboubakar Zubeir Ali ametoa pongezi hizo jana jioni tarehe 24 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam katika futari iliyoandaliwa na Rais Magufuli na akatumia nafasi hiyo kuwasihi Waislamu na watanzania wote kwa ujumla kukataa vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani. 

“Niwahusie ndugu zangu watanzania wote, kwamba amani ni kitu muhimu tuitunze amani tuliyokuwa nayo, tuienzi amani tuliyonayo, na hapo tutakuwa tunaisadia serikali na tutakuwa tunamsadia Mhe. Rais katika kuilinda amani” Amesema Mufti Mkuu. 

Gerson Msigwa 
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
25 Juni, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akikagua kituo cha mawasiliano ya polisi (Call centre) katika kituo cha Kati jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa Kitaifa wa Kituo cha Mawasiliano cha Jeshi la Polisi. .Pamoja naye ni Waziri wa mambo ya Ndani Mhe Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Ndani Meja Jenerali Projest Rwegasira, IGP Ernest manu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda na viongozi wengine wa sekta ya umma na binfasi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akizindua Kituo kidogo cha Polisi kinachohamishika wakati wa uzinduzi wa Kitaifa wa Kituo cha Mawasiliano cha Jeshi la Polisi (Call Centre) katika viwanja vya Biafra jijini Dar es salaam.. Pamoja naye ni Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa mambo ya Ndani Mhe Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu kiongozi Mhe. John Kijazi, IGP Ernest manu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda na viongozi wengine wa sekta ya umma na binfasi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akizindua Kituo kidogo cha Polisi kinachohamishika wakati wa uuzinduzi wa Kitaifa wa Kituo cha Mawasiliano cha Jeshi la Polisi (Call Centre) katika viwanja vya Biafra jijini Dar es salaam.. Pamoja naye ni Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa mambo ya Ndani Mhe Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu kiongozi Mhe. John Kijazi, IGP Ernest manu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda na viongozi wengine wa sekta ya umma na binfasi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akikagua kituo cha mawasiliano ya polisi (Call centre) katika kituo cha Kati jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa Kitaifa wa Kituo cha Mawasiliano cha Jeshi la Polisi. .Pamoja naye ni Waziri wa mambo ya Ndani Mhe Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Ndani Meja Jenerali Projest Rwegasira, IGP Ernest manu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda na viongozi wengine wa sekta ya umma na binfasi. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hongera za kipekee ziwaendee wizara ya mambo ya ndani chini ya Mh Mwigulu Nchemba na Kwa jeshi LA polisi kupitia Kwa IGP na Kwa wadhamini wote.
    Pamoja na hayo yote kuna mambo mengi yanahitaji kuangaliwa katika jeshi LA polisi Kwa mfano MTU anapata na matatizo anaenda polisi kureport lakini pamoja na matatizo Bado wapelelezi wanakua wanahitaji pesa kama rushwa kukufanyia kazi,its totally not acceptable,naomba muangalie hilo,pia Kwa upande wa wezi wanapokamatwa na kuachwa huru kirahisi inakua inaleta Imani potofu kua majambaz yanafahamika na polisi lakini hayawezi shughulikiwa.

    Polisi ni sehemu ambayo ni salama na ya msaada Kwa RAIA,lakini inapokua karaha na si rafiki Kwa watu wenye matatizo.MTU unaibiwa Gari unafika report polisi then polisi wanaweka mazingira tofauti inaumiza sana ,naombeni muangalie hilo tafadhali

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...