Madaktari Bingwa Sita kutoka nchini China   wameanza kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi mbalimbali katika Jimbo la Musoma Vijijini ikiwa ni mwaliko wa Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni  Waziri wa  Nishati na Madini,  Profesa Sospeter Muhongo. 
Madaktari hao wameanza kutoa huduma hiyo katika Zahanati ya Mugango iliyopo kijiji cha Nyangoma wilayani Musoma ambapo Huduma hiyo ya afya inatolewa kwa Awamu ya Pili  baada ya huduma kama hiyo kutolewa na Madaktari wengine kutoka China mnamo mwezi Machi mwaka huu. 
Akizindua matibabu hayo ya Awamu ya Pili, Profesa Muhongo alisema kuwa wananchi hao hawatalipia  matibabu hayo yanayotolewa tarehe 25 na 26 Juni, 2016   na kwamba Madaktari hao wamebobea katika magonjwa ya Wanawake, Watoto, Meno, Vinywa, koo, macho, kisukari, presha, tumbo na kufanya upasuaji wa uvimbe kichwani na tumboni.
“Nimeleta rafiki zangu kutoka China na watawatibu kwa muda wa siku Mbili lakini pia Madaktari hawa wanaojitolea wamekuja na rafiki zao ambao wameleta, kalamu na vitabu vya Sayansi, Hisabati, na Kiswahili, kwa ajili ya kugawa katika shule Tano za Msingi, pamoja na mipira ambayo itagaiwa katika shule hizo na timu za mipira za hapa kijijini,” alisema Profesa Muhongo. 
Naye Mwakilishi kutoka Ubalozi wa China hapa nchini, Bwana Zhang Biao, alisema kuwa uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi za Tanzania na China ndiyo umechangia kwa kiasi Madaktari hao kutoka China kuja nchini kutoa huduma hizo za matibabu. 
“Ushirikiano wetu unazidi kupanuka na wanachi wengi wa China wanakuja Tanzania kufanya biashara, hali kadhalika wananchi wa Tanzania wanaenda China kwa masuala ya Bishara na Utalii, kwa ushirikiano huu tutazidi kupanuka hata kiuchumi,” alisema Zhang. 
Alisema kuwa hadi sasa kuna Madaktari zaidi ya 20 kutoka China wanaotoa huduma za matibabu nchini ambao wapo katika mikoa ya Dar es Salaam, Tabora, Mara na Dodoma na hii yote inatokana na urafiki na undugu uliopo katika ya nchi hizo mbili.
Wakati huohuo Profesa Muhongo amezindua ugawaji wa vitabu zaidi ya 22,000 katika Shule za Msingi na Sekondari za Jimbo la Musoma vijijini ambapo uzinduzi huo ameufanya katika shule ya msingi Kwibara kata ya Mugango. 
Katika uzinduzi huo, Profesa Muhongo alisema kuwa Jimbo hilo lina shule za msingi 108 na Sekondari 20 ambapo kila shule ya msingi itapata maboksi ya vitabu mawili huku kila shule ya sekondari ikipata maboksi 16. 
Profesa Muhongo alisema kuwa vitabu hivyo ameletewa na Rafiki zake kutoka nchini Marekani ambapo thamani ya vitabu hivyo ni Dola za Marekani 250,000, “ lengo langu ni kuhakikisha kuwa wananchi katika Jimbo hili mnaelimika kwa kujenga utamaduni wa kujisomea, hivyo vitabu hivi hata wananchi mnakaribishwa kuja kuvisoma,”alisema Profesa Muhongo. 
Aidha, Profesa Muhongo alisema kuwa katika  kutimiza ahadi zake,  amewapeleka wananchi hao Gari aina ya Canter  Kwa ajili ya kusaidia katika Shughuli za Misiba, ujenzi wa Shule, Maabara na vituo Vya Afya, pia  ametimiza  ahadi ya gari ya kubebea wagonjwa ambapo mwezi Machi, 2016 alilikabidhi Gari hilo la wagonjwa katika Hospitali ya Murangi.
Akiwaeleza wananchi Mipango ya kuendeleza huduma za Afya katika Jimbo la Musoma Vijijini, alisema kuwa " Leo nawataarifu kuwa baada ya wiki 2 nitaleta gari nyingine 4   za kubebea wagonjwa na zitagawanywa katika
Zahanati ya Kurugee, -Kata ya Bukumi, Zahanati ya Masinono-Kata ya Bugwema, Zahanati ya Mugango-Kata ya Mugango na Zahanati  ya Nyakatende-Kata ya Ifulifu.
Vilevile alisema kuwa bado kuna vitabu vingine vinavyoendelea kuletwa nchini ambapo Awamu nyingine ya 3 inategemewa kufika Mwezi Agosti, 2016 ambavyo pia atavigawa katika Majimbo mengine ya Mkoa wa Mara bila kubagua itikadi ya Chama kwani wananchi wote wana haki ya kupata maendeleo, aidha Awamu ya 4 ya vitabu inategemewa kufika mwezi Octoba, 2016.

 Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na wananchi katika Zahanati ya Mugango kijiji cha Nyangoma wilayani Musoma wakati alipofika katika Zahanati hiyo kuzindua huduma ya matibabu inayotolewa na Madaktari Bingwa Sita kutoka nchini China ikiwa ni mwitikio wa mwaliko uliotolewa na Profesa Muhongo.  
 Mwakilishi kutoka Ubalozi wa China hapa nchini, Zhang Biao akizungumza na wananchi katika Zahanati ya Mugango kijiji cha Nyangoma wilayani Musoma wakati Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto kwa Bw. Zhang) alipofika katika Zahanati hiyo kuzindua huduma ya matibabu inayotolewa na Madaktari Bingwa Sita kutoka nchini China ikiwa ni mwitikio wa mwaliko uliotolewa na Profesa Muhongo
 Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika picha  ya Pamoja na Madaktari Bingwa kutoka nchini China na baadhi ya Wananchi waliofika katika Zahanati ya Mugango kijiji cha Nyangoma wilayani Musoma,  wakati Profesa Muhongo alipofika katika Zahanati hiyo kuzindua huduma ya matibabu inayotolewa na Madaktari hao Bingwa Sita kutoka nchini China.
 Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (aliyeshika kipaza sauti) akiwa katika picha  ya pamoja na baadhi ya Wanafunzi na Walimu wa Shule ya Sekondari Kwibara, iliyopo katika Jimbo hilo, mara baada ya kuzindua ugawaji wa vitabu zaidi ya 22,000 katika Shule za Msingi na Sekondari za Jimbo la Musoma vijijini.
 Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika picha  ya pamoja na baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kwibara, iliyopo katika Jimbo hilo, mara baada ya kuzindua ugawaji wa vitabu zaidi ya 22,000 katika Shule za Msingi na Sekondari za Jimbo la Musoma vijijini. Maboksi yanayoonekana ni ya baadhi ya vitabu hivyo vinavyosambazwa katika Jimbo hilo.
Katibu Mkuu wa Timu ya Madaktari kutoka China waliopo nchini, Song Tao,  akizungumza na wananchi katika Zahanati ya Mugango kijiji cha Nyangoma wilayani Musoma wakati Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto kwa Song Tao) alipofika katika Zahanati hiyo kuzindua huduma ya matibabu inayotolewa na Madaktari Bingwa Sita kutoka nchini China ikiwa ni mwitikio wa mwaliko uliotolewa na Profesa Muhongo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...