Ndugu Wandishi wa Habari, 
Mabibi na Mabwana,
Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru nyote hasa waandishi wa habari kwa kutenga muda wenu na kujumuika nasi kwa lengo la kutangaza rasmi kuanza kutumika kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 ambayo ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali  la tarehe 14/08/2015 na kupewa Na. 328. Pia Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, 2015 ambayo  ilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe hiyo hiyo na kupewa Na.329.

Ndugu Wananchi,
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo ya kisasa inayotumika kubeba na kusafirisha ujumbe, taarifa, takwimu, picha na sauti kwa kutumia njia na mifumo mbalimbali ya mawasiliano iliyopo, kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine au eneo moja kwenda eneo lingine kwa uharaka, ufasaha, kwa wakati na kwa kiwango cha ubora ule ule bila kujali umbali na mipaka iliyopo ya kijiografia. Matumizi ya TEHAMA yameleta mafanikio katika kuharakisha, kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuchangia kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini. Mathalani, wananchi walio wengi sasa wanapata huduma mbalimbali za kifedha, kulipia huduma (leseni, kodi, Ankara), matumizi ya mitandao ya kijamii, barua pepe na huduma mtandao kama vile Serikali mtandao, afya mtandao, kilimo mtandao, biashara mtandao, Elimu mtandao, n.k

Ndugu Wananchi
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo kumekuwepo na changamoto mbalimbali kama vile wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, uvujaji wa taarifa, kusambazwa kwa ujumbe wa matusi, picha chafu, uchochezi, udhalilishaji, vitisho kupitia mitandaoni. Vile vile kuna watu wachache ambao wanaharibu miundombinu ya mawasiliano, kwa mfano wanakata mkongo wa Taifa wa mawasiliano na mikongo mingine ya mawasiliano na hili lina athari kubwa sana kwa nchi yetu na kwa nchi za jirani ambazo zimeunganishwa kwenye mkongo wa Taifa wa mawasiliano.

Ndugu Wananchi 
Mtakumbuka kuwa, mnamo tarehe 1 Aprili 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya Mwaka 2015. Pamoja na masuala mengine, sheria hizi zinabainisha makosa, kutambua ushahidi wa nyaraka za kielektroniki na pia kuainisha adhabu zinazokwenda pamoja na makosa mbalimbali ya kimtandao. Sheria hizi ni muhimu sana na zina manufaa makubwa kwenye jamii yetu haswa katika nyakati hizi ambapo matukio ya uhalifu wa mtandao yamekuwa yakiongezeka na kukosekana kwa Sheria hizi kumefanya Wananchi kutokuwa na mahala pa kukimbilia pale wanapokumbana na uhalifu kupitia mitandaoni.

Aidha, ninatambua ya kuwa Sheria hizi zimepokelewa kwa hisia tofauti kutokana na uelewa mdogo kwa wengi wetu kuhusu sheria hizi. Vilevile ni ukweli usiopingika kuwa kumekuwa na tafsiri hasi kwa baadhi ya wananchi juu ya maudhui ya sheria hizi na kuzifanya zitafsiriwe kama kandamizi zaidi kitu ambacho ni tofauti na dhana na maudhi ya sheria hizi.  

Kwa kutambua hilo, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia mara baada ya kupitishwa kwa SHERIA  hizi  ilianza kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kuwa na mikutano na makundi mbalimbali ya watekelezaji wa Sheria hizi ili kuwajengea uelewa ikiwemo Jeshi la Polisi, Waendesha Mashtaka, Wachunguzi, Wapelelezi, Mahakimu na Majaji kuhusu Sheria hizi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani Bara na Zanzibar. Aidha, ili kuhakikisha kuwa usimamizi na utekelezaji wa Sheria hizi unakwenda vizuri, Wizara itaendelea kuwajengea uelewa Wadau mbalimbali. 

Ndugu Wananchi
Tanzania siyo nchi ya kwanza kutunga sheria kama hizi. Kuna nchi mbalimbali duniani ambazo zimetunga sheria kama hizi, kwa mfano nchi ya Uingereza (UK Computer Misuse Act, 1990), India (IT Act, 2000), Malaysia (Computer Crime Act), Uganda (Computer Misuse Act, 2010), Korea ya Kusini (Information and Communications Network Act na Information and Communication Infrastructure Protection Act), Singapore (The Computer Misuse and Cyber security Act), Mauritius (Computer Misuse and Cybercrime Act, 2003), Marekani (Computer Fraud and Abuse Act, 1984) na nyingi nyenginezo. 

Ndugu Wananchi,
Serikali baaada ya kujiridhisha kuwa maandalizi yote muhimu ikiwemo elimu kwa umma na kujenga uelewa kwa watekeleza wa sheria hizi yamefanyika. Sasa, Sheria hizi zitaanza kutumika rasmi tarehe 01/09/2015. 

Kwa hivyo, natoa rai na wito kwa wananchi wote kuwa tuzingatie “Matumizi Salama na sahihi ya Huduma za Mawasiliano na Mtandao kwa manufaa ya kila  mmoja  na kwa maendeleo ya Taifa letu. Mitandao ikitumiwa vema ina faida kubwa sana katika jamii yetu.

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
 Wanahabari kazini wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika rasmi kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na ya Miamala ya Kieletroniki za mwaka 2015. 
 Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa (Mb), akiongea na waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika rasmi kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na ya Miamala ya Kieletroniki za mwaka 2015. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bwana John Mngodo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...