Na Felix Mwagara, Mishamo

ZOEZI la ugawaji wa vyeti vya uraia wa Tanzania kwa waliokuwa Wakimbizi wa Burundi zaidi ya 152,572 walioingia nchini mwaka 1972 linatarajiwa kumalizika wiki hii katika Makazi ya Mishamo mkoani Katavi.

Wakimbizi hao ambao waliomba uraia wa Tanzania mwaka 2008 na kupewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2010, sasa watakuwa raia halali wa Tanzania kwa kuwa na uwezo wa kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo za Udiwani na Ubunge.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa vyeti hivyo, Mkuu wa Makazi ya Mishamo, Fredrick Nisajile alisema ugawaji wa vyeti hivyo ulianza Novemba 24 mwaka jana, katika Makazi ya Katumba yaliyopo mkoani Katavi, ambapo watu 56,554 walipewa vyeti vya uraia na baadaye zoezi la ugawaji likahamia katika Makazi ya Ulyankulu mkoani Tabora, ambapo watu 43,453 tayari wamepewa vyeti hivyo.

Nisajile alisema katika makazi yake ya Mishamo ambapo ugawaji wa vyeti hivyo unaendelea na unatarajiwa kumalizika ifikapo Aprili 30 mwaka huu, ambapo katika makazi hayo zaidi ya raia wapya 52,565 wanatarajiwa kupewa vyeti vyao.

“Mpaka leo hii (jana) katika makazi haya ya Mishamo kama unavyoshuhudia ndugu mwandishi umati wa watu wakizidi kuingia katika kituo hiki, mpaka sasa tayari tumegawa vyeti 131,351 kwa raia hawa wapya, na tunatarajia ifikapo wiki ijayo Aprili 30 tutakuwa tumemaliza ugawaji wa vyeti hivi katika vijiji vyote, na zaidi ya raia wapya 152,572 katika Makazi ya Katumba, Ulyankulu na Mishamo watakuwa wamepewa vyeti hivi na zoezi litakuwa limekamilika” alisema Nisajile.

Alisema Serikali ndiyo inatoa vyeti hivyo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), ambapo wote kwa pamoja wamejipanga kikamilifu ili ugawaji huo unamalizika salama na kwa umakini wa hali ya juu.

Hata hivyo, Nisajile alisema kuwa, makazi yake ya Mishamo yana vijiji 16, hivyo kabla ya kuanza kugawa vyeti hivyo, huwa wanatoa elimu kwa kuwahamasisha wakazi wa kijiji ambacho kinatarajia siku ya pili yake kwenda kugawiwa vyeti hivyo. Alisema katika uhamasishaji huo, yeye Mkuu wa Makazi anaambatana na Maafisa Uhamiaji na UNHCR ili waweze kuhamasisha mambo mbalimbali kuhusiana na umuhimu wa vyeti hivyo.

Aliongeza kuwa, vyeti hivyo vinatolewa kwa mtu mmoja mmoja ambapo raia mpya anatakiwa aje na karatasi ya uthibitisho wa picha za wanafamilia ili kuiwezesha Serikali na UNHCR kutambua kabla ya kutoa cheti kwa wahusika hao na kila anayepewa cheti hicho anatakiwa kusaini.

Zoezi la ugawaji wa vyeti vya uraia kwa raia hao wapya lilikuwa la miezi mitano, ambapo lilianza Novemba 24 mwaka 2014, na Aprili 30 wiki hii, linatarajiwa kukamilika.
Afisa Uhakiki, Neema Chilipweli (kushoto) akiihakiki familia ya Yohanna Bukuru (watatu kulia), pamoja na mkewe na watoto wao sita kutoka Kijiji cha Kapemba, Kata ya Mishamo, wilayani Mpanda Vijijini, Mkoa wa Katavi, ikiwa ni hatua ya awali ya uhakiki ili familia hiyo iweze kupewa vyeti vya uraia wa Tanzania. Zaidi ya watu 152,572 katika Makazi ya Mishamo, Katumba na Ulyankulu waliokuwa wakimbizi wa Burundi wa mwaka 1972 walioomba uraia 2008 na kupewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2010, wanastahili kupokea vyeti hivyo kama raia wapya wa Tanzania. Hata hivyo, Makazi ya Katumba na Ulyakulu tayari wamekamilisha zoezi la ugawaji wa vyeti hivyo, na sasa ni zamu ya raia wapya wa Makazi ya Mishamo ambapo wiki hii zoezi la ugawaji wa vyeti hivyo nchini, linatarajiwa kukamilika. Serikali ya Tanzania inashirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) katika ugawaji wa vyeti hiyo. Picha na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...