Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imetiliana saini ya makubaliano na Kampuni ya UDA Rapid Transit kuendesha huduma ya usafiri ya mradi huo katika kipindi cha mpito. 
Katika mkataba huo wa miaka miwili kampuni hiyo itatakiwa kununua mabasi 76 yenye urefu wa mita 12 na 18 ili kuanza kutoa huduma hiyo katika barabara za mradi jijini Dar es Salaam miezi minne kuanzia sasa. 
Wakati DART ikiwakilishwa na Mtendaji Mkuu wake, Bi. Asteria Mlambo, kampuni hiyo iliwakilishwa na Bw.Robert Kisena na Bw. Sabri Mabruki na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Saidi Meck Sadiki na viongozi wengine. 
Bw. Kisena ni Mwenyekiti wa Simon Group Ltd, kampuni inayoendesha Usafiri Dar es Salaam (UDA). 
Akizungumza katika halfa ya utiaji saini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Bi. Ghasia alisema tukio hilo ni la kihistoria katika mchakato wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka. 
“Tumefikia hatua nzuri kwa nchi yetu kuwa serikali imeweza kushirikiana vyema na wadau wa usafiri kupata kampuni ya kuendesha huduma ya usafiri kipindi cha mpito,”alisema. 
Alisema pamoja na kwamba mradi mzima haujakamilika, serikali imeamua kuanza na huduma ya mpito katika barabara ya Kimara hadi Kivukoni ambayo imekamilika kwa asilimia 90 na kuwa sasa kazi inayofanyika ni ya kuweka taa za barabarani. 
Alifafanua kuwa usafiri katika barabara hiyo utakuwa wa uhakika na wa kisasa kwa vile basi moja la urefu wa mita 18 litakuwa na uwezo wa kubeba watu 150 wakati yale ya mita 12 yatakuwa na uwezo wa kubeba abiria 80 kila moja. Kampuni ya UDA Rapid Transit imeundwa na Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) na wamiliki wa daladala. 
Waziri huyo aliitaka kampuni hiyo kuendelea kujenga mshikamano ili kupata uwezo wa kushindana katika zabuni ya kuendesha huduma ya kudumu ya mradi huo baada ya kipindi cha mpito kuisha. Mwakilishi wa Kampuni ya UDA Rapid Transit ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA), Bw. Mabruki alisema wao wamejipanga kutoa huduma nzuri ya usafiri kipindi cha mpito. 
“Tunaishukuru serikali kwa kutuwezesha wadau wa usafiri kufikia tulipo,” alisema. Alisisitiza kuwa katika kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa kampuni yao itakuwa imeleta mabasi mawili yenye sifa zinazotakiwa kwa ajili ya kufundishia madereva na hadi kufikia Septemba 15 mwaka huu mabasi yote 76 yatakuwa yameshaletwa. 
Pia alisema kampuni yao inatarajia kujisajili katika soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kuwapa fursa wananchi kununua hisa katika kampuni hiyo na kuwa sehemu ya wamiliki. 
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Sadiki alisema mradi huo ni mkubwa hivyo wananchi pamoja na madereva wanatakiwa kuyathamini basi hayo na kulinda miundombinu yake. Alikemea tabia ya udokozi kama ilivyojitokeza kwa taa za barabarani na mifuniko na vyuma mbalimbali vya mradi na wizi uliofanyika katika reli ya Kati wakati treni ya kisasa ilipoanza safari ya kwanza ya uzinduzi wake. 
 Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Bw. Jumanne Sagini alisema huduma ya mabasi hayo katika kipindi cha mpito itapunguza adha ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam ambapo hali imekuwa mbaya. 
“Jiji hili linakua kwa haraka na mahitaji ya usafiri yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa,” alisema. 
Alisema inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2025 jiji hili litakuwa na wakazi milioni 11.5 hivyo uboreshaji miundombinu ni jambo lisiloepukika.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya kutiliana saini ya makubaliano ya kuanza kwa utekelezaji wa kipindi cha mpito cha huduma ya mabasi yaendayo haraka mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Kampuni ya UDA Rapid Transit itaendesha mradi huo.  Kulia kwake ni Kamishna wa Kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam, Suleiman Kova na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Saidi Meck Sadiki.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bi. Asteria Mlambo (wa pili kushoto), na wawakilishi wa kampuni ya UDA Rapid Transit, Bw. Robert Kisena (wa tatu kulia) na Bw. Sabri Mabruki (wa kwanza kushoto) wakitiliana saini ya makubaliano ya kuanza kwa utekelezaji wa kipindi cha mpito cha huduma ya mabasi yaendayo haraka mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Pamoja na viongozi wengine wanaoshuhudia ni waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi.Hawa Ghasia (wa pili kushoto waliosimama); Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Bw. Jumanne Sagini (kushoto) na Kamishna wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova (kulia).
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bi. Asteria Mlambo (wa pili kushoto) akibadilishana hati na mwawakilishi wa kampuni ya UDA Rapid Transit, Bw. Robert Kisena (wa pili kulia) kuhusu makubaliano ya kuanza kwa utekelezaji wa kipindi cha mpito cha huduma ya mabasi yaendayo haraka kuanzia mwezi wa tisa mwaka huu.  Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Kushoto ni muwakilishi mwingine wa kampuni hiyo, Bw. Sabri Mabruki.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...