Gati ya Mafia iliyofunguliwa rasmi na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete mjini Mafia leo
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kuzindua rasmi Gati la Mafia iliyojengwa wilayani Mafia leo.Kushoto ni Waziri wa Uchukuzi Dkt.Harrison Mwakyembe. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Mafia Mheshimiwa Abdul Karim Shah,Wantatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi.Mwantum Mahiza na kulia ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitembea juu ya Gati la Mafia lenye urefu wa kilometa moja na nusu muda mfupi baada ya kulifungua rasmi mjini Mafia leo.Wengine katika picha kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi.Mwantumu Mahiza, wa pili kushoto ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete,wa nne kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mafia Bi. Sauda Mtondoo na kulia ni mbunge wa Mafia Mhe.Abdul Karim Shah. 
Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuachana na hulka ya kukejeli jitihada za maendeleo na kujenga fitina kuhusu miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa baadhi ya Watanzania, badala ya kuunga mkono jitihada za maendeleo, wanapiga kasi mpya ya kurudi nyuma kwa kupinga na kukejeli miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza leo, Alhamisi, Oktoba 3, 2013, Kisiwani Mafia wakati alipoanza ziara ya siku tano kukagua shughuli za maendeleo na kufungua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Chuo cha Ufundi, Tereni, nje ya mji mkuu wa Mafia wa Kilindoni, Rais Kikwete ameimwagia sifa Mfuko wa Maendeleo ya Mafia (MIDEF) ambao umefanikisha mambo makubwa ya maendeleo katika Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo hicho ambacho kitagharimu kiasi cha sh. bilioni 5.33 na kuchukua wanafunzi 400 kitakapokamilika. Chuo hicho pia kitakuwa na sehemu ya Chuo cha Michezo – Sports Academy.
Mbali na ujenzi wa chuo hicho, MIDEF imejenga shule ya sekondari ya bweni, imeunga mkono shule za sekondari za kata za Serikali kwa kuzipa kompyuta na madawati, inatoa mikopo ya maendeleo kwa wananchi, imetoa zana za kazi kwa taasisi za Serikali na imesimamia kupatikana kwa fedha za kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Mafia kupitia Mamlaka ya Kusambaza Umeme Vijijini (REA).
Kwenye mradi wa kusambaza umeme vijijini, kwa mfano, MIDEF imechangia kiasi cha Sh. Milioni 500 katika mradi ambao utagharimu Sh. Bilioni tano.
Rais Kikwete amewaambia wananchi wa Mafia: “Jitihada hizi za MIDEF lazima ziungwe mkono. Sina maneno mazuri ya kuwaambieni kuwa kama hamtaunga mkono jitihada hizo mtakuwa na matatizo, tena matatizo makubwa sana. Mtakuwa mnafikia kwa kasi mpya ya kurudi nyuma.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nasema hivyo kwa sababu sisi Watanzania kazi yetu imekuwa ni kujenga fitina, kubeza na kukejeli jitihada za maendeleo. Hiyo ndiyo hulka yetu kujenga fitina kuhusu miradi ya maendeleo.”
“Tunashangaza sana. Mtu anayekuhubiria upate maendeleo unamwona mtu mbaya, lakini mtu anayekuhubiria usipate maendeleo unamuona mtu mzuri na mwema. Tabia hii ndiyo naiita ya kupiga kasi mpya ya kurudi nyuma,” amesema Rais Kikwete.
Katika ujenzi wa Chuo hicho cha Ufundi, Serikali imechangia kwa kutoa ardhi ya kujenga chuo hicho katika eneo la Tereni na kukamilika kwa Chuo hicho kuitaiwezesha Tanzania kuongeza idadi ya vyuo vya ufundi nchini. Kwa sasa kuna vyuo vya ufundi 742 vyenye wanafunzi 145,510, kati ya hivyo 17 vikiwa vya Serikali, na vilivyobakia vikiwa vya watu na taasisi binafsi.
Rais Kikwete ambaye ameshinda siku nzima katika Wilaya hiyo ya Mafia amerejea Dar Es Salaam jioni ya leo na kesho atafanya ziara ya Wilaya ya Mkuranga.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.


3 Oktoba, 2013

 Vijana wa Scout wakimvisha skafu Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mafia leo asubuhi ambapo alifungua uwanja wa ndege wa Mafia na kuzindua Gati la Mafia.Rais Kikwete yupo katika ziara ya kikazi ya mkoa wa Pwani.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunua kitambaa kuashiria kuzindua rasmi uwanja wa Ndege Mafia uliojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na mfuko wa Millenium Challenge Corporation(MCC),Kulia ni Mratibu wa shughuli za MCC nchini Bwana Bernard Mchomvu na katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi Mwantumu Mahiza na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mafia muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi Gati la Mafia leo asubuhi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Hongereni sana wana midef.ila picha ya juu naona Mbunge wa Mafia kama hana confidence.hajiamini.
    Mdau Lewisham UK.

    ReplyDelete
  2. jamani hiyo inaitwa gati kweli?

    ReplyDelete
  3. Mdau wa KWANZA wa Lewisham -UK,

    Mbunge wa Mafia jamaa namkubali sana, Mhe. Shah Mbunge wa Mafia anayo confidence kwa kuwa yeye ni Mtu Makini sana.

    Nakumbuka kipindi cha Mafuriko Jijini Dar alikuwepo Jijini na alitoa Mchango Mkubwa sana kuokoa watu na Maafa ya maji, Mhe.Shah ni Mfano wa Kuigwa !

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...